Alhamisi 18 Juni 2026 - 21:54
Damu ya Mashahidi Iliuvunja Ushawishi wa Marekani na Uzayuni

Hawza/ Sheikh Khalid Al-Mulla, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Ahlus-Sunnah nchini Iraq, katika mkutano wa kimataifa wenye anuani ya “Watoto Mashahidi, Kushindwa kwa Tawwla ya Marekani na Kuamka kwa Umma wa Kiislamu”, alisisitiza kuwa; damu ya mashahidi iliuvunja ushawishi wa Marekani na Uzayuni, na ikasababisha wimbi la mwamko wa Kiislamu na kibinadamu duniani kote.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Khalid Al-Mulla, Rais wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Ahlus-Sunnah Iraq, katika hotuba yake kwenye mkutano wa kimataifa wenye anuani ya “Watoto Mashahidi, Kushindwa kwa Tawala ya Marekani na Kuamka kwa Umma wa Kiislamu”, ulioratibiwa na Majma‘ ya Kimataifa ya Qadimun na kurushwa kupitia kituo cha televisheni cha Al-Kawthar, aliipongeza hali ya mapambano ya muqawama na ushindi wa mataifa dhidi ya ubeberu na tamaa za kutawala wengine, na kusema: “Leo tumekusanyika katika mazingira yanayoashiria kuvunjika kwa vikwazo na kuporomoka kwa nguvu na ushawishi wa Uzayuni; ushawishi ambao umevunjwa na mujahaidina, wapiganaji wa muqawama pamoja na vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Akinukuu Aya Tukufu isemayo:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْيَهُودَ وَالنَّصَارَى أَوْلِيَاءَ...﴾

alisema: “Aya hii inaelekezwa kwa waumini na kwa uwazi kabisa inatahadharisha dhidi ya kuingia katika ushirikiano na mikondo inayojipanga dhidi ya Umma wa Kiislamu. Leo tunashuhudia kuwa madola ya kibeberu pamoja na utawala wa Kizayuni yameungana kwa ajili ya kuendeleza maslahi yao ya pamoja dhidi ya mataifa ya eneo hili.”

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Ahlus-Sunnah Iraq, akizungumzia shambulio la Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisema: “Marekani daima imejitahidi kulazimisha utawala wake si tu katika nyanja za kisiasa na kiuchumi, bali pia katika maeneo ya kitamaduni na hata kidini. Katika kila kipindi imekuwa ikijaribu, kupitia majina na miradi mbalimbali, kuunda tafsiri ya dini inayokwenda sambamba na maslahi yake.”

Alisisitiza: “Watu wote wanaounga mkono au kuhalalisha uvamizi na jinai za Marekani na utawala wa Kizayuni wanashiriki jukumu la damu ya mashahidi waliouawa kishahidi nchini Iran, Lebanon, Yemen, Iraq na maeneo mengine ya muqawama.”

Sheikh Khalid Al-Mulla, akirejelea kuuawa kishahidi kwa makamanda na raia wa Iran pamoja na tukio la kusikitisha la shule ya Minab lililosababisha kuuawa kishahidi kwa idadi kubwa ya watoto na wanafunzi, alisema: “Japokuwa jinai hizi zilisababisha huzuni kubwa kwa Umma wa Kiislamu, adui alipuuzia ukweli mmoja mkubwa, nao ni kwamba damu ya mashahidi ndiyo yenyewe itakuwa sababu ya mwamko na kuinuka kwa mataifa.”

Aliongeza: “Kilichotokea katika vita hivi ni kuvunjika kwa hadhi na nguvu za Marekani pamoja na uwezo wake wa kijeshi katika eneo hili; kwa namna ambayo vifaa vyake vya kijeshi, manowari zake, makombora yake na uwezo wake wa kivita havikuweza kuvunja azma ya mataifa yanayopinga dhulma.”

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Ahlus-Sunnah Iraq pia alizungumzia wimbi kubwa la mshikamano wa kimataifa na wananchi wa Iran, akisema: “Msaada na mshikamano haukuishia katika nchi za Kiislamu pekee, bali hata katika nchi mbalimbali za Ulaya, Marekani, Australia na Kanada tulishuhudia watu wakionesha masikitiko yao na mshikamano wao na waathirika wa vita hivi.”

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alieleza kuhusu uungaji mkono wa wananchi na viongozi wa kidini katika ulimwengu wa Kiislamu, akisema: “Nchini Iraq, misimamo ya Mar'ajii wa kidini na mbele yao Ayatullah Sayyid Ali Sistani, pamoja na taarifa za wanazuoni wa Ahlus-Sunnah Iraq, vilikuwa ni ishara ya mshikamano wa Umma wa Kiislamu na wananchi wa Iran, misaada ya wananchi na misafara ya kuunga mkono pia ilionesha kuwa kusimama pamoja na taifa lililovamiwa kumekuwa jukumu kubwa la Kiislamu.”

Sheikh Khalid Al-Mulla, katika hitimisho la hotuba yake, alitaja matokeo mawili muhimu ya matukio haya:

Kwanza, kuvunjika kwa ushawishi, kiburi na madai ya ubora wa Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni mbele ya muqawama wa mataifa.

Pili, kuibuka kwa wimbi la mwamko wa Kiislamu na kibinadamu ambalo damu ya mashahidi, hususan watoto mashahidi na waathirika wengine wa vita, imelichochea katika sehemu mbalimbali za dunia.

Mwishoni, huku akiwashukuru waandaaji wa mkutano huo, vyombo vya habari vilivyofikisha ujumbe huu kwa ulimwengu na mataifa yanayounga mkono muqawama, alisifu uimara wa wananchi wa Iran pamoja na msaada wa mataifa ya Iraq, Misri, Algeria na mataifa mengine huru duniani, na akaelezea matumaini yake kwamba; ushindi wa mwisho dhidi ya dhulma, uvamizi na tamaa za kutawala wengine vitapatikana.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha